Rais Tshisekedi: Katiba ni 'dhaifu' inahitaji kufanyiwa marekebisho
Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, idadi ya mihula ya urais haitabadilishwa, lakini wapinzani wake wanasema ana nia ya kuwania muhula wa tatu.
Pamoja na hayo Rais Félix Tshisekedi, anasema kuwa katiba ya nchi hiyo inapaswa kurekebishwa kwa sababu ina "udhaifu" fulani.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Tshisekedi kuzungumza hadharani kuhusu suala hilo lenye utata, baada ya chama chake cha UDPS kuanzisha kampeni mwezi huu ya kufanyia marekebisho katiba.
Katika hotuba yake kwa lugha ya Lingala, Rais Tshisekedi alisema kuwa katiba inapaswa kurekebishwa kulingana na "hali halisi ya Kongo".
Tshisekedi alisema kuwa "hatua hii haitaathiri idadi ya mihula katika uchaguzi wa rais" lakini wapinzani wake wanasema kuwa ni njia ya kujaribu kufanya kampeni kwa ajili ya muhula wa tatu.
Wanamtaka aachie madaraka wakati muhula wake wa pili alioapishwa Januari Mosi mwaka huu utakapomalizika.
Hayo yanajiri katika halii ambayo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa usalama mashariki mwa nchin hiyo.
Wimbi la mashambulizi mapya ya waasi wa M23 na ADF linaendelea kuwatesa wananchi wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) huku mapigano baina ya wanajeshi wa serikali na waasi wa makundi hayo mawili yakiendelea.