Balozi wa Sudan ailaani Israel kwa kuchochea moto wa vita nchini mwake
Balozi wa Sudan mjini Tehran ameulaani utawala wa Kizayuni kwa kuchochea moto wa vita nchini mwake na kusema kuwa, Israel na makundi yanyopigana kwa niaba ya madola ya kigeni ndiyo sababu ya maafa yanayoendelea hivi sasa Sudan.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Abdul Aziz Hassan Saleh Taha alisema hayo jana mbele ya waandishi wa habari hapa Tehran na kuongeza kuwa, kinachotokea Sudan hivi sasa ni jinai kubwa ambayo imenyamaziwa kimya au kupotoshwa na vyombo vya habari. Jinai zote dhidi ya binadamu zinafanyika hivi sasa Sudan. Mnachokishuhudia leo hii ni sehemu ndogo tu ya jinai kubwa zinazofanywa na wanamgambo na waasi wanaosaidiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Balozi wa Sudan mjini Tehran ameongeza kuwa, wanamgambo nchini Sudan wamefanya mauaji makubwa mno dhidi ya raia. Wanamgambo hao huwa wanachimba mahandaki na kuwafukia raia wanaowaua, hawajali watoto wala vijana wala vizee na hawajali wanawake wala wanaume. Hadi sasa wameshawateka nyara maelfu kwa maelfu ya raia na kuwafanyia ukatili usioelzeka.
Balozi Abdul Aziz Taha ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni ndicho chanzo cha vita vinavyoendelea hivi sasa nchini kwake Sudan. Ameongeza kuwa, magenge ya waasi na ya kigaidi yako chini ya Israel tangu siku ya mwanzo ya vita. Magenge hayo yanatokea katika nchi za kama Niger na Chad na wanapigana bega kwa bega na waasi na kufanya jinai za kutisha dhidi ya raia nchini Sudan.