Iran: Uingiliaji wa Marekani wakusudia kuchochea vurugu na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135234-iran_uingiliaji_wa_marekani_wakusudia_kuchochea_vurugu_na_ugaidi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu Iran imekemea vikali kauli za kuingilia na za upotoshaji zilizotolewa na maafisa wa Marekani kuhusu hali za ndani ya Iran, ikisema matamshi hayo yanaakisi uhasama wa kudumu wa Washington dhidi ya taifa hili na yamelenga kuibua machafuko na hali ya kutokuwa na usalama nchini.
(last modified 2026-01-07T23:37:08+00:00 )
Jan 07, 2026 23:37 UTC
  • Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
    Jengo la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu Iran imekemea vikali kauli za kuingilia na za upotoshaji zilizotolewa na maafisa wa Marekani kuhusu hali za ndani ya Iran, ikisema matamshi hayo yanaakisi uhasama wa kudumu wa Washington dhidi ya taifa hili na yamelenga kuibua machafuko na hali ya kutokuwa na usalama nchini.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, wizara hiyo ilisisitiza kuwa misimamo ya Marekani haitokani na hofu ya dhati kwa wananchi wa Iran, bali imefungamana na sera ya “shinikizo la juu kabisa, vitisho na kuingilia” mambo ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, msimamo huo wa kuingilia unakusudia kuchochea vurugu na ugaidi, na kudhoofisha uthabiti wa taifa.

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa, kwa mujibu wa Katiba ya Iran, maandamano ya amani yanatambuliwa, na serikali inashughulikia madai halali ya wananchi kwa mujibu wa sheria.

Iliongeza kuwa, ingawa Iran inachukua hatua za kupunguza matatizo ya kiuchumi, sehemu kubwa ya changamoto hizo zinatokana na vita vya kiuchumi na kifedha vilivyoanzishwa na Marekani dhidi kupitia vikwazo visivyo halali na visivyo na haki.

Wizara ilibainisha kuwa hatua za Washington dhidi ya Iran hazikomei katika shinikizo la kiuchumi pekee, bali zinajumuisha pia vita vya kisaikolojia, kampeni za vyombo vya habari, kusambaza taarifa za uongo, vitisho vya kuingilia kijeshi, na uchochezi wa vurugu na ugaidi.

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa mwenendo wa aina hiyo unapingana na misingi ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kanuni za lazima za sheria za kimataifa, na nguzo za mfumo wa kimataifa wa haki za binadamu.

Ikikumbusha historia ndefu ya uhasama na kuingilia kwa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran, wizara ilirejelea mapinduzi ya mwaka 1953 dhidi ya serikali iliyochaguliwa kidemokrasia wakati huo, msaada wa Marekani kwa utawala wa Kiba’ath wa Iraq katika vita vilivyodumu kwa miaka minane dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, ushiriki pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita visivyo halali vilivyoanzishwa mjini Tel Aviv mwezi Juni, na pia kuwekewa vikwazo vya upande mmoja.

Taarifa hiyo ilikumbusha kuwa hatua hizi za uadui zinabainisha wajibu wa Umoja wa Mataifa na taasisi za kimataifa kulinda sheria za kimataifa, hususan kuhusu heshima kwa mamlaka ya kitaifa na kutokujihusisha katika mambo ya ndani ya mataifa mengine.

Taarifa hiyo ilihitimisha kwa kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itakabiliana na uingiliaji wa mambo yake ya ndani, kwa kutegemea urithi wake wa Kiislamu na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, na haitaruhusu sera za Marekani kudhoofisha mamlaka yake ya kitaifa, uhuru wake, na heshima yake.