Ethiopia yazishutumu balozi za kigeni kwa kuvuruga uchumi, yatishia kuchukua hatua
(last modified Mon, 04 Nov 2024 06:27:30 GMT )
Nov 04, 2024 06:27 UTC
  • Ethiopia yazishutumu balozi za kigeni kwa kuvuruga uchumi, yatishia kuchukua hatua

Waziri Mkuu wa Ethiopiam, Abiy Ahmed amezishutumu balozi za kigeni kwa kujihusisha na magendo ya fedha za kigeni akidai kuwa balozi hizo zinaibia Ethiopia rasilimali zake.

Mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, Abiy Ahmed alizindua sera ya mageuzi ya uchumi iliyojulikana kwa kifupi kwa jina la HGER 2.0, kwa shabaha ya kushughulikia matatizo ya kimuundo ya uchumi, ikiwa ni pamoja na mzigo wa madeni, mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira pamoja na kuleta utulivu wa soko la fedha za kigeni nchini Ethiopia.

Abiy Ahmed amesema wakati akilihutubia Bunge la Ethiopia kwamba, kuna baadhi ya balozi ambazo zinaiba rasilimali za nchi yake na kufanya biashara ya fedha za kigeni kwa njia ya magendo.

Waziri Mkuu huyo ameelezea kukasirishwa sana na jambo hilo na ametishia kuzichukulia hatua kali balozi hizo kwa kuendesha ubadilishaji haramu wa fedha unaoyumbisha uchumi wa Ethiopia.

Amesema: "Hadi sasa tumekuwa wavumilivu. Hatutaki kuharibu uhusiano wetu mzuri na nchi nyingine. Hata hivyo, tunataka uhusiano unaoheshimu sheria za nchi yetu." 

Shutuma hizi zimekuja huku Ethiopia ikiwa katikati ya utekelezaji wa sera ya mageuzi ya uchumi yenye lengo la kutatua changamoto za muda mrefu za kiuchumi nchini humo.

Benki na mashirika ya ubadilishanaji fedha yenye leseni sasa yanatoa viwango rasmi, lakini juhudi hizo zinakwamishwa na ubadilishaji fedha nje ya mkondo huo na kuleta changamoto katika juhudi za serikali Ethiopia za kuleta utulivu katika soko lake la fedha za kigeni.