Somalia yaitaka Ujerumani isiwafukuze wahajiri Waafrika
Somalia imeitaka Ujerumani isitishe mpango wake wa kuwafukuza Waafrika wakiwemo Wasomali nchini humo.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alikutana na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Berlin siku ya Jumatano kujadili ushirikiano kuhusu kufukuzwa kwa wahamiaji Wasomali.
Msemaji wa serikali ya Somalia Farhan Mohamed Jimale alichapisha taarifa kwenye X na kusema kwamba Mohamud alimwambia Olaf Scholz kwamba hakuna haja ya kuwarejesha nyumbani kwa lazima Wasomali wanaoishi Ujerumani.
Mohamud alisema milango iko wazi kwa watu wa Somalia ambao hawana tena haki ya kupata hifadhi na wanataka kurejea Somalia kwa hiari.
Rais wa Somalia amesema: "Wanakaribishwa kurudi katika nchi yao, kuungana na familia zao ambapo wanaweza kuchangia maendeleo ya nchi na kuwa sehemu ya maendeleo ya pamoja ya Somalia."
Jumla ya Wasomali 65,000 wanaishi Ujerumani.
Ujerumani inalaumiwa kwa kukiuka haki za binadamu katika mpango wake huo wa kuwatimua wakimbizi kutoka Somalia ambao wanasema wanahofia maisha yao wakirejea nyumbani. Misimamo ya serikali ya Ujerumani dhidi ya wakimbizi imechangiwa pia na kuenea makundi ya wazungu wabaguzi wenye misimamo mikali dhidi ya wageni.