Jeshi la Sudan: Tumeua wapiganaji 150 wa RSF Magharibi mwa nchi
Jeshi la Sudan (SAF) limetangaza kwamba limeua wapiganaji 150 wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika vita vilivyozuka baina ya pande hizo mbili, huko El Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini la magharibi mwa Sudan.
Kamanda wa Kitivo cha 6 cha Jeshi la Sudan SAF huko El Fasher ametangaza habari hiyo kwa kusema: "Vikosi vyetu vimepigana katika vita kwa zaidi ya saa mbili kusini-mashariki mwa El Fasher."
"Kambi kadhaa za wanamgambo zimetekwa hadi sasa, huku maadui waliouawa wakikadiriwa kufikia 150," imeongeza taarifa hiyo ikibainisha kuwa, vikosi vya SAF vinaendelea kusonga mbele kwa kasi kubwa.
Hadi wakati tunaandaa habari hii, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vilikuwa havijatoa taarifa yoyote kuhusu madai hayo.
Sudan imekumbwa na mzozo mbaya wa uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya mwezi Aprili 2023.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mgogoro huo mbaya umeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 24,850 na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni 14 kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.