Polisi wa Afrika Kusini wanapanga kuwaondoa wachimba madini haramu chini ya ardhi
Msemaji wa Polisi ya Afrika Kusini, Athlenda Mathe, amesema kuwa wataalamu wa uokoaji wamekutana ili kutekeleza operesheni ya kuwatafuta wachimbaji haramu katika mgodi uliotelekezwa. Haya yanajiri huku kukiwa na mzozo kati ya wachimba migodi na polisi ya Afrika Kusini ambao umeendelea kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Maafisa wa Afrika Kusini wanasema kuwa, wachimba madini hao haramu hawajakwamwa chini ya mgodi bali wamekataa kutoka katika mgodi huo uliotelekezwa kwa hofu ya kukamatwa na maafisa wa polisi wanaowasubiri.
Msemaji wa Polisi ya Afrika Kusini ameongeza kuwa, tunaendelea na zoezi la kuwaondoa ndani ya mgodi kama tulivyoagizwa lakini kwa kuchukua tahadhari za usalama.
Wakati huo huo, Mahakama Kuu ya Afrika kusini imeahirisha kesi iliyowasilishwa na wachimba mgodi hao wakitaka waruhusiwe kutoka chini ya ardhi bila ya kutiwa nguvuni.
Juzi Jumatatu, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini alisema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya operesheni iliyopewa jina la "Vala Umgodi" kote nchini humo ambayo inaendelea kupata mafanikio katika kukabiliana na shughuli haramu za uchimbaji madini nchini Afrika Kusini.
Ramaphosa ameeleza kuwa shughuli za wachimbaji haramu zimeathiri uchumi wa jamii na usalama wa watu binafsi nchini Afrika Kusini. Hata hivyo Rais Ramaphosa ametaka kadhia hiyo ya wachimba madini haramu itatuliwe kwa njia ya amani.