Bara la Afrika laongoza katika mauaji ya wanawake duniani
(last modified Tue, 26 Nov 2024 13:17:01 GMT )
Nov 26, 2024 13:17 UTC
  • Bara la Afrika laongoza katika mauaji ya wanawake duniani

Imebainika kuwa wanawake na wasichana 140 walifariki dunia kila siku duniani kote mwaka 2023 wakiwa mikononi mwa watu wa karibu, ikimaanisha kuwa mwanmake mmoja aliuawa katika kila dakika 10, na kwa mantiki hiyo ni jumla ya wanawake 85,000 waliouawa huku bara la Afrika likiongoza.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Jumatatu na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la masuala ya wanawake, UN Women na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za kulevya na Uhalifu, (UNODC).

Ripoti hiyo imetolewa kwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 tangu kupitishwa kwa Siku ya Kimataifa ya kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake, na inaangazia janga la mauaji ya wanawake na kutoa wito kwa hatua za dharura zichukuliwe kukabili janga hilo.

Mauaji ya wanawake yanavuka mipaka, hali ya kiuchumi, kijamii na utamaduni. Hata hivyo kiwango au ukubwa wake unatofautiana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bara la Afrika lilivunja rekodi ya kuwa na viwango vya juu vya wanawake kuuawa na wapenzi wao au mwanafamilia. Wanawake 21,700 waliuawa Afrika mwaka wa 2023, ikifuatiwa na bara la Amerika na kisha Oshenia.

Barani Ulaya na Amerika, idadi kubwa ya wanawake waliuawa na wapenzi wao, ikiwa ni asilimia 64 na 58 mtawalia ya matukio yote ya mauaji.

Tofauti kwa Afrika na Asia, wanawake waliuawa zaidi na wanafamilia badala ya wapenzi wao, na hivyo kuonesha tofauti za tamaduni na mienendo ya kijamii inavyoendana na ubaguzi dhidi ya wanawake.