Libya yataka kufutwa uanachama wa utawala wa Israel katika Umoja wa Mataifa
Libya imetaka kufutwa uanachama wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa na kuhuishwa sura ya saba ya Hati ya Baraza la Usalama dhidi ya utawala huo unaotekeleza mauaji ya kimbari.
Ashraf Ali Hamed Mwakilishi wa Libya katika kikao cha Kamati Maalumu ya Masuala ya Kisiasa na Kuondoa Ukoloni ya Umoja wa Mataifa ameashiria jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina na kusisitiza kuwa ipo haja kwa utawala wa Israel kuwekewa vikwazo vya kimataifa kufuatia jinai za kivita unazofanya dhidi ya Wapalestina.
Ali Hamed amelaani kwa maneno makali mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.
Mwakilishi wa Libya ameashiria matatizo yanayowasibu wananchi wa Palestina na kusema: Mbali na kuuawa shahidi watu zaidi ya elfu 44, kujeruhiwa na kupotea makumi ya maelfu ya watu; miundombinu muhimu ya eneo hilo imebomolewa na aghalabu ya wakazi wa Gaza wamelazimika kukubali mateso ya kuwa wakimbizi.

Mwakilishi wa Kudumu wa Libya katika Umoja wa Mataifa amesisitiza uungaji mkono wa nchi yake kwa wananchi wa Palestina na kusema: Mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina yanapasa kukomeshwa haraka iwezekanavyo na kutekelezwa maazimio yote katika uwanja huo na raia hao kurejeshewa haki zao walizoporwa.