Kiongozi wa upinzani Kongo ahukumiwa jela miaka miwili
Mahakama ya Congo Brazzaville imemuhukumu kifungo cha miaka miwili jela Paulin Makaya, kiongozi wa upinzani kwa tuhuma za kuchochea machafuko ya ndani nchini humo.
Paulin Makaya amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela kwa tuhuma za kuratibu maandamano bila kibali hapo mwaka jana 2015. Makaya anayeongoza chama cha Muungano kwa ajili ya Kongo, alisema kuwa atakata rufaa kupinga hukumu dhidi yake. Kadhalika mahakama hiyo imemtaka kulipa kiasi cha Euro 3800.
Mawakili wa upande wa utetezi waliitaja hukumu hiyo kuwa isiyo ya haki na inayokinzana na sheria. Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka 2014, Paulin Makaya na baada ya kipindi cha miaka 17 ya kubaidishwa alirejea nchini Congo Brazzaville na kujihusisha na masuala ya siasa.
Kwa mujibu wa ripoti, maandamano hayo yalifanyika mwezi Oktoba mwaka jana katika kupinga hatua ya serikali ya kuitisha kura ya maoni nchini humo. Kura hiyo ya maoni ilihitimisha ukomo wa mihula miwili ya uongozi na hivyo kutoa fursa kwa Rais Denis Sassou Nguesso kugombea tena katika uchaguzi wa mwezi Machi mwaka huu ambapo pia aliibuka kuwa mshindi.