Ronnie Kasrils: Umewadia wakati wa kufutwa kura ya turufu ambayo inailinda Israel
Ronnie Kasrils aliyekuwa mmoja wa viongozi wa Harakati ya Ukombozi, ambaye ni mfuasi wa dini ya Kiyahudi na Mzungu wa Afrika Kusini, ameeleza kuwa Israel inaeneza uharibifu katika eneo Asia Magharibi, sio tu kwa kufanya jinai ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, bali kwa kuishambulia Lebanon na kuvamia ardhi yake, na mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi ya Syria, Iraq na Yemen.
Kasrils ameongeza kuwa njia pekee ya kukomesha uharibifu huo ni kuinyima mashine ya kijeshi ya Israel silaha zinazotolewa na Marekani, Ujerumani, Uingereza na nchi nyingine zinazoisaidia Israel kufanya uhalifu huo.
Ronnie Kasrils ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali ya Afrika Kusini amesema kuwa, njia ya kusimamisha mtiririko wa silaha kuelekea Israel ni kupitia Umoja wa Mataifa ambao unadhalilishwa na Washington na Tel Aviv. Amesema, hatua hiyo ni jukumu la jamii nzima ya kimataifa kwa sababu tawala hizo zinakiuka sheria za kimataifa, haki za binadamu na maazimio yote ya kimataifa.
Ameashiria unafiki na sera za kindumakuwili za nchi za Magharibi ambazo zimeungana kuihami na kuisaidia kwa hali na mali Ukraine, huku zikiunga mkono dola linalotenda jinai kama Israel.
Amesisitiza kuwa, watu wote nchini Afrika Kusini, serikali na chama tawala, katika ngazi za uongozi na mashinani, wanaunga mkono Muqawama na mapambano dhidi ya Wazayuni wa Kizayuni na Marekani.
Ronnie Kasrils amesema, umewadia wakati wa kufutwa kura ya turufu ambayo inailinda Israel.
Kasrils amesisitiza: “Tunaona kwamba tangu karne ya saba, Uislamu na Mtume wake, Muhammad, kiongozi, kamanda wa kijeshi na kiongozi wa serikali, aliweka mafundisho madhubuti ya jinsi ya kukabiliana na adui, ikiwa ni pamoja na kukataza kuwaua wanawake, watoto na majeruhi, na kulindwa maeneo ya kidini,” akiashiria tofauti ya ajabu kwa kulinganisha mafundisho hayo na sheria za Israel, Marekani, Ufaransa, Ujerumani ya Kinazi na Uingereza, suala ambalo linaweka wazi kwa nini wanafumbia macho jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina na eneo zima na Asia Magharibi.