Makumi ya watu wafa maji, makumi hawajulikani waliko Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120290-makumi_ya_watu_wafa_maji_makumi_hawajulikani_waliko_kongo_dr
Boti iliyokuwa imejaa watu ilipinduka kwenye mto katikati mwa Kongo jana Jumanne, na kuua takriban watu 25, wakiwemo watoto. Makumi ya abiria wengine wa boti hiyo wametoweka na hawajulikani waliko.
(last modified 2024-12-18T04:06:29+00:00 )
Dec 18, 2024 04:06 UTC
  • Makumi ya watu wafa maji, makumi hawajulikani waliko Kongo DR

Boti iliyokuwa imejaa watu ilipinduka kwenye mto katikati mwa Kongo jana Jumanne, na kuua takriban watu 25, wakiwemo watoto. Makumi ya abiria wengine wa boti hiyo wametoweka na hawajulikani waliko.

Boti hiyo iliaminika kuwa na zaidi ya abiria 100 baada ya kuondoka katika mji wa Inongo, kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Kinshasa. Ilipinduka mita mia kadhaa ikiwa safarini kando ya Mto Fimi; huo ukiwa mkasa wa mpya zaidi wa ajali za boti kuikumba nchi ya Kongo.

Operesheni ya kutafuta manusura ilikuwa ukiendelea jana huku wasiwasi ukiongezeka kwamba idadi ya waliofariki dunia inaweza kuwa kubwa zaidi.

"Boti ilipakiwa kupita kiasi kwenye paa na watu wasiopungua 25 wameokolewa hadi sasa," amesema kamishna wa Mto Inongo, David Kalemba.

Boti hiyo iliyopinduka pia ilisheheni bidhaa. Mkazi wa eneo hilo, Alex Mbumba amesema: "Miongoni mwa waliofariki dunia ni watoto, lakini ni vigumu kutoa idadi kamili ya vifo kwa sasa, kwa sababu boti hiyo ilikuwa na abiria wengi." 

Ajali hiyo ya jana Jumanne ni ya nne mwaka huu katika jimbo la Maï-Ndombe, eneo linalozungukwa na mito ambapo wengi wanategemea usafiri wa majini.