Waasi wazidi kusonga mbele mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado linaendelea kukumbwa na vitendo vya ghasia zinazofanywa na waasi na sasa wakiwa wameingia katika mji wa Butembo na kwingineko ambako tayari wameteka vijiji zaidi ya 10.
Inaonekana kuwa waasi wanazidi kusonga mbele hatua ambayo inaliweka jeshi la nchi hiyo kupungukiwa nguvu ya kupambana nao.
Ingawa walinda amani wa SADC na MONUSCO wako katika maeneo ya DRC lakini hali ya uasi bado inaongezeka.
Wakati huo huo, wakulima wengi wanaokwenda mashambani mashariki mwa DRC wanalindwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa umekuwa chini ya uangalizi mkubwa kwa miaka mingi huku mzozo mashariki mwa nchi baina ya makundi ya uasi, na vikosi vya ulinzi na wanamgambo wengine ukiendelea.
Majuzi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilibadilisha msimamo wake kuhusu mchakato wa kuondooka nchini humo kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO).
Mwezi Januari mwaka huu Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendelezo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC dhidi ya waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.