Hofu yatanda Msumbiji kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi
Msumbiji inajiandaa kwa maandamano zaidi huku matokeo ya mwisho ya uchaguzi unaodaiwa na wapinzani kuwa ulikuwa na utata yakitarajiwa kutangaza kabla yya Jumatatu ijayo.
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane ametishia kuitisha uasi wa nchi nzima kama Baraza la Katiba litaidhinisha matokeo ya awali ambayo yalimuweka katika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa Oktoba 9 akishindwa na mgombea wa chama tawala cha Frelimo.
Ripoti kutoka Msumbiji zinasema kuwa, mrengo wa upinzani umejiandaa kuanzisha maandamano ya nchi nzima kupinga matokeo endapo Mahakama ya Katiba itaidhinisha matokeo yanayompa ushindi mgombea wa chama tawala.
Maandamano yalianza nchini Msumbiji Oktoba 24 mwaka huu baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo kumtangaza mgombea wa chama tawala cha Mozambique Liberation Front (Frelimo) Daniel Chapo kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais baada ya kujinyakulia asilimia 70 ya kura zilizopigwa, huku Mondlane akishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 20.
Maandamano hayo yameendelea licha ya kutolewa mwito wa kufanyika mazungumzo ya kuhitimisha mzozo huo.
Takriban watu 90 wameuawa na wengine 340 kujeruhiwa tangu ghasia za baada ya uchaguzi kuikumba Msumbiji mwezi Oktoba mwaka huu.