Serikali ya Kenya kufuatilia mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofadhili ugaidi
-
Raymond Omollo
Serikali ya Kenya imetangaza kuuwa, inayafuatilia mashirika yasiyo ya serikali yanayotumia vibaya fedha za wafadhili kusaidia shughuli haramu ikiwemo ugaidi.
Raymond Omollo Katibu Mkuu wa Wizara ya Usalama wa Ndani ametoa onyo kali kwa mashirika yasiyo ya serikali dhidi ya kutumia vibaya fedha za wafadhili kusaidia shughuli haramu, ikiwa ni pamoja na ugaidi.
Amesema baadhi ya mashirika yanatumiwa katika ubadilishaji wa siri wa matumizi ya fedha zinazokusudiwa kwa madhumuni halali. Afisa huyo wa serikali ya Kenya amebainisha kuwa, baadhi ya mashirika yamesajiliwa kwa miradi tofauti lakini yanatumiwa kama njia za kuhamisha fedha haramu kusaidia shughuli za kigaidi.
Amehimiza kukuza uwajibikaji na imani kubwa kati ya mashirika yasiyo ya serikali katika jumuiya ya wafadhili, taasisi za fedha na umma, kwamba fedha zinawafikia walengwa waliokusudiwa.
Amesema kuwa serikali imeimarisha ufuatiliaji wa fedha za mashirika yasiyo ya serikali hata kama baadhi yanasalia kusita kufichua vyanzo vyao vya ufadhili.
Haya yanajiri katika hali ambayo, jopo kazi la kimataifa la uangalizi wa fedha kulingana na viwango vya kimataifa dhidi ya utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi Financial Action Task Force (FATF) limeiweka Kenya kwenye orodha ya mataifa yanayofuatiliwa kutokana na mapungufu katika kushughulikia utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi.
Miongoni mwa masuala yaliyoainishwa ni pamoja na, kushindwa Kenya kushtaki kesi za utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi, kutokuwepo kwa kanuni za muongozo wa biashara ya sarafu mtandao yaani (cryptocurrencies) na mashirika yasiyo ya serikali, na uangalizi dhaifu katika sekta ya mali isiyohamishika kama vile ujenzi.