Rais wa Ufaransa akiri, Afrika imebadilika
-
Emmanuel Macron
Wakati Ufaransa imepoteza kambi zake nyingi za kijeshi barani Afrika, sasa rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron, katika safari ya kimyakimya kwenye kituo cha mwisho cha operesheni za nchi hiyo huko Djibouti, amekiri kwamba: Afrika inabadilika kwa sababu maoni ya umma na Serikali yamo katika hali ya kubadilika, hivyo nafasi yetu barani Afrika pia itabadilika.
Katika safari hiyo, Macron amekiri kwamba kambi ya kijeshi ya Ufaransa nchini Djibouti inaweza kuwa na nafasi muhimu zaidi na kukiri kuwa: Ufaransa inalazimika kubadilisha mantiki yake ya zamani ya kuwa na kambi nyingi za kijeshi barani Afrika. Macron pia ametangaza kuwa majukumu ya kambi ya kijeshi ya Ufaransa huko Djibouti yataarifishwa upya na kusema kambi hizi zinapaswa kutumika kama sehemu ya utumiaji nguvu katika baadhi ya misheni za Ufaransa barani Afrika.
Safari ya Macron nchini Djibouti imefanyika baada ya Ufaransa kupoteza kambi zake nyingi za kijeshi katika nchi tofauti za Afrika, hasa katika eneo la Sahel na Afrika Magharibi. Kwa hakika nchi mbalimbali za Kiafrika kama vile Mali, Burkina Faso, Niger na hivi karibuni Chad ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimefunga kambi za kijeshi za Ufaransa na kuyafukuza majeshi ya nchi hiyo katika ardhi zao.

Kufukuzwa vikosi vya majeshi ya Ufaransa katika nchi tofauti za Kiafrika kunafanyika licha ya kwamba nchi mbalimbali za bara hilo zilikuwa chini ya udhibiti wa Ufaransa kwa miaka mingi. Kwa hakika, jinai zilizofanywa na Ufaransa wakati ilipoikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria na kisha kuwauwa Waalgeria, na kuhusika nchi hiyo katika mauaji ya kimbari ya Rwanda na Cameroon kamwe haviwezi kufutika katika kumbukumbu ya kihistoria ya watu wa bara la Afrika.
Licha ya ukweli kwamba Paris ililazimishwa kutambua uhuru wa nchi makoloni yake ya zamani kama vile Algeria katika miongo kadhaa iliyopita kutokana na mwamko na mapambano ya mataifa ya Kiafrika, lakini kamwe haikuondoka kikamilifu barani Afrika. Paris imekuwapo katika nchi nyingi za bara hilo katika fremu ya ukoloni mamboleo ikitumia visingizio mbalimbali kama vile kurejesha usalama, kupambana na ugaidi na kusaidia kuboresha hali ya kiuchumi.
Bara la Afrika lina umuhimu maalumu kwa Ufaransa katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijeshi. Kwa mfano, katika nyanja za kiuchumi, hadi 2020, makampuni ya Kifaransa yalikuwa yakihodhi karibu uzalishaji wa rasilimali za madini katika makoloni ya zamani ya nchi hiyo kama Niger na Mali, kwa kadiri kwamba sehemu kubwa ya mahitaji ya uranium inayotumiwa kama fueli katika vinu vya nyuklia vya Ufaransa ilikuwa ikitolewa katika nchi kama vile Niger.

Katika sekta ya masuala ya kijeshi, vikosi vya Ufaransa vimekuwepo katika nchi tofauti za Kiafrika na mara nyingi vimekuwa vikisimamia kamandi za kijeshi. Katika muktadha huu, tunaweza kutaja uwepo wa jeshi la Ufaransa katika nchi kama Mali, Niger, Ivory Coast na Chad kwa kisingizio cha kusaidia kuimarisha usalama na amani na kupambana na ugaidi katika miaka 10 iliyopita, na Ufaransa ilikuwa na kambi rasmi za kijeshi katika baadhi ya nchi hizo.
Ingawa katika miaka kumi iliyopita, Ufaransa katika mfumo wa ukoloni mamboleo, ambao ulijaribu kuibakisha nchi hiyo barani Afrika kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia visingizio kama kuchangia misaada ya kifedha, kutekeleza miradi ya kiuchumi na kibiashara, kutoa mikopo, kujenga viwanda na vituo vya kijeshi, lakini hulka ya kikoloni na uhalifu wa nchi hiyo havikusahauliwa na umma wa Waafrika, kiasi kwamba katika miaka michache iliyopita, nchi nyingi za Kiafrika zilitaka rasmi kukomesha uwepo wa kijeshi wa Ufaransa katika bara lao na kufukuzwa vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo. Mali, Burkina Faso, Niger, na Chad ni miongoni mwa nchi ambazo zimeyatimua rasmi majeshi ya Ufaransa na kuchukua udhibiti wa mambo yao wenyewe. Suala hili limewachukiza sana viongozi wa Ufaransa na hata nchi nyingine za kikoloni za Ulaya. Pamoja na hayo wakoloni hao wa zamani wanapasa kukubali hali halisi ya dunia ya sasa. Ni kwa msingi huo ndiyo maana Catherine Colonna, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ufaransa, amekiri rasmi kwamba enzi ya ukoloni wa nchi hiyo barani Afrika zimekwisha na kwamba wimbi la chuki dhidi ya Ufaransa limeshamiri barani Afrika.
Pamoja na hayo Wafaransa na wakoloni wengine wanapaswa kutambua kuwa Waafrika hawawachukii Wafaransa kama Wafaransa, bali wanachukia ukoloni, ubabe, kuporwa mali na rasimali zao, kudharauliwa na kudunishwa na kutazamwa kama watu wa daraja la pili na pengine la tatu na nne...