Jul 27, 2016 02:42 UTC
  • UN: Mzunguko wa pesa haramu watishia uchumi wa Afrika

Kamisheni ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA) imetahadharisha kuwa, mzunguko wa pesa haramu katika akthari ya nchi za Afrika unatishia ukuaji wa uchumi wa bara hilo.

Abdalla Hamdok, Naibu Katibu Mkuu na Mchumi Mkuu wa kamisheni hiyo amesema asilimia 60 ya fedha hizo zilizochumwa kwa njia za kutiliwa shaka na haramu zinatokana na miamala ya kibishara kati ya nchi za Afrika na mashirika ya kimataifa yanayokwepa kulipa kodi, huku asilimia 35 ya fedha hizo zikitumika katika masuala ya uhalifu. Mchumi huyo ameongeza kuwa, fedha zinazopotea katika mzunguko haramu wa pesa kwa ajili ya kukwepa kulipa kodi Afrika zinapindukia fedha ambazo nchi za bara hilo zinapokea kutoka kwa wafadhili kila mwaka ambazo ni zaidi ya dola bilioni 80 za Marekani.

Thabo Mbeki, Mweyekiti wa Jopo la Maendeleo-Endelevu la Afrika

Ripoti ya mwaka jana 2015 ya Jopo la Maendeleo-Endelevu la Afrika linaloongozwa na rais wa zamani wa Afrika Kusini Tyabo Mbeki ilisema kuwa, fedha haramu zinazozunguka barani Afrika kwa mwaka ni zaidi ya dola bilioni 50 za Marekani.

Ufuaji wa fedha waathiri pakubwa chumi za nchi za Afrika

Kamisheni ya Umoja wa Afrika hivi karibuni ilisema kuwa, iwapo nchi za Afrika zitafanikiwa katika kupambana na mzunguko wa pesa haramu sambamba na kukabiliana na ufuaji wa fedha, basi bara hilo litakuwa katika nafasi nzuri ya kustawi kiuchumi na kuondokana na utegemezi wa nchi wafadhili na taasisi za kifedha duniani.

Tags