UN: Wakenya 42,000 walikuwa wakimbizi 'bandia' Dadaab
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, Wakenya 42,000 wamekuwa wakijifanya wakimbizi katika kambi ya Dadaab kwa shabaha ya kufaidika na misaada ya kibinadamu.
Duke Mwancha, msemaji wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema uchunguzi wao umefichua kuwa, maelfu ya Wakenya walijisajili kuwa wakimbizi katika kambi ya Dadaab ili wapate chakula na huduma za bure. Ameongeza kuwa, Umoja wa Mataifa unahitajia dola milioni 115.4 za Marekani ili kufanikisha mpango wa kuwarejesha wakimbizi hao katika nchi zao.
Mapema mwezi huu, oparesheni ya kuwarejeshwa makwao wakimbizi wa kambi ya Dadaab ilianza licha ya kuwepo juhudi za kimataifa za kutaka kuzuia zoezi hilo. Imepangwa kuwa kambi hiyo ambayo inahesabiwa kuwa kubwa zaidi ya wakimbizi dunia, itakuwa imefungwa kikamilifu kufikia mwezi Mei mwaka 2017. Nusu ya wakimbizi wa kambi ya wakimbizi ya Dadaab ni Wasomali waliokimbilia Kenya katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Kambi hiyo iko umbali wa kilomita mia moja kutoka kwenye mpaka wa nchi mbili za Kenya na Somalia.
Viongozi wa Kenya walitangaza kuwa wamelazimika kuifunga kambi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi, kimazingira na kiusalama.