Katika ujumbe wa Mwaka Mpya, Ramaphosa ataka kukomeshwa vita Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120876-katika_ujumbe_wa_mwaka_mpya_ramaphosa_ataka_kukomeshwa_vita_ghaza
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kwa mara nyingine tena ametoa mwito wa kukomeshwa haraka vita dhidi ya wananchi wa Ghaza. Amesema hayo kwenye ujumbe wa Mwaka Mpya aliotoa jana Jumanne.
(last modified 2025-01-01T03:09:45+00:00 )
Jan 01, 2025 03:09 UTC
  • Katika ujumbe wa Mwaka Mpya, Ramaphosa ataka kukomeshwa vita Ghaza

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kwa mara nyingine tena ametoa mwito wa kukomeshwa haraka vita dhidi ya wananchi wa Ghaza. Amesema hayo kwenye ujumbe wa Mwaka Mpya aliotoa jana Jumanne.

Katika sehemu moja ya ujumbe wake huo, Rais Ramaphosa amesema: "Wakati mgogoro wa Mashariki ya Kati ukiendelea na mauaji ya umati yakiendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu wa Ghaza, sisi pia tunaendelea kutoa mwito wa kukomesha vita mara moja." Aidha kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa Afrika Kusini itaendelea kusimama kidete kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina.

Akizungumzia vita vinavyoendelea na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, Ramaphosa amesema: "Kama ambavyo sisi tulipata uhuru wetu kupitia uungaji mkono na mshikamano wa watu na mataifa mengi duniani, na sisi pia tunaendelea kusimama katika mshikamano na watu wanaodhulumiwa kwenye sehemu mbalimbali za dunia."

Afrika Kusini ilifungua keshi dhidi ya Israel kutokana na jinai za kutisha zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Ilifungua kesi hiyo katika mahakama ya kimataifa ya jinai yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi mwishoni mwa mwaka juzi 2023. Nchi kadhaa duniani zimejiunga na kesi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambayo ilianza kusikilizwa hadharani mwezi Januari mwaka jana 2024.

Jeshi la Israel linaendelea kufanya mauaji ya umati dhidi ya wananchi wa Ghaza na hadi hivi sasa limeshaua shahidi zaidi ya Wapalesitna 45,500, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto watoto wadogo, tangu Oktoba 7, 2023. Mwezi Novemba mwaka jana 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICJ) ilitoa hati za kutiwa mbaroni waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita,Yoav Gallant kutokana na uhalifu mkubwa wa kivita waliofanya dhidi ya wananchi wa Ghaza.