Wafuasi wa chama tawala Burundi wakosolewa kwa kuhusika na jinai
Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limelaani vitendo vya ukatili vinavyofanywa na baadhi ya wafuasi wa chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo imekosoa vikali vitendo vinavyofanywa na vijana wa chama hicho tangu kuibuka mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo hapo mwezi April mwaka jana hadi sasa. Kwa mujibu wa shirika hilo, baadhi ya jinai hizo zimetekelezwa na polisi. Hii ni katika hali ambayo mwezi Januari mwaka huu Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa kama hiyo dhidi ya chama tawala nchini humo.
Zeid Ra'ad Al Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa umoja huo alikosoa vitendo visivyo vya kimaadili ambavyo vimetekelezwa na maafisa usalama wa serikali ya Bujumbura. Kwa mujibu wa Al Hussein hadi wakati huo, kulikuwa na kesi 13 za vitendo vilivyo kinyume na akhlaqi dhidi ya wanawake, ambavyo viliripotiwa kutokea katika maeneo ya wapinzani nchini humo. Burundi ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwezi Aprili mwaka jana baada ya chama tawala CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea katika uchaguzi uliopita.
Katika vurugu hizo zaidi ya watu 500 wameuawa na zaidi ya wengine laki mbili kuwa wakimbizi.