Watu 20 wapoteza maisha katika ajali ya ndege Sudan Kusini
Kwa akali watu 20 wameaga dunia katika ajali ya ndege iliyotokea leo Jumatano nchini Sudan Kusini.
Radio Miraya ya Umoja wa Mataifa imetengaza habari hiyo na kuongeza kuwa, ndege hiyo iliyokuwa imebeba abiria 21 imeanguka muda mfupi baada ya kupaa angani katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Unity.
Waziri wa Habari katika jimbo la Unity, Gatwech Bipal amesema ndege hiyo ilianguka katika uwanja wa ndege wa Kisima cha Mafuta cha Unity asubuhi ilipokuwa ikielekea mji mkuu Juba.
Bipal amesema abiria hao walikuwa wafanyakazi wa Kampuni ya Mafuta ya Greater Pioneer Operating Company (GPOC), muungano unaojumuisha Shirika la Taifa la Petroli la China na Shirika la Petroli la Nile linalomilikiwa na serikali.

Anasema miongoni mwa watu waliofariki dunia kwenye ajali hiyo ni raia wawili wa China na mmoja wa India. Bipal hakutoa maelezo zaidi kuhusu chanzo cha ajali hiyo.
Ripoti za vyombo vya habari hapo awali ziliweka idadi ya waliopoteza maisha kuwa 18, lakini Bipal ameiambia Reuters kwamba majeruhi wawili walifariki dunia baadaye. Mtu mmoja amenusurika kwenye ajali hiyo.
Ajali nyingi za ndege zimetokea katika Sudan Kusini iliyokumbwa na vita katika miaka ya hivi karibuni. Mnamo Septemba 2018, watu 19 walifariki dunia wakati ndege ndogo iliyokuwa imebeba abiria kutokaJuba kuelekea mji wa Yirol ilipoanguka.