Umoja wa Mataifa wasimamisha kwa muda utoaji misaada ya kibinadamu Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12208-umoja_wa_mataifa_wasimamisha_kwa_muda_utoaji_misaada_ya_kibinadamu_nigeria
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, umesimamisha kwa muda shughuli zake za utoaji misaada ya kibinaadamu nchini Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 29, 2016 03:44 UTC
  • Umoja wa Mataifa wasimamisha kwa muda utoaji misaada ya kibinadamu Nigeria

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, umesimamisha kwa muda shughuli zake za utoaji misaada ya kibinaadamu nchini Nigeria.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetangaza kuwa, sababu ya kusimamisha shughuli zake za utoaji misaada ya kibinadamu nchini Nigeria ni kushambuliwa kwa misafara yake na watu wenye silaha.

Wakimbizi kaskazini mashariki mwa Nigeria

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, misafara yake ya upelekaji misaada ya kibinadamu imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na watu wenye silaha kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imeeleza kuwa, kabla ya kuendelea tena na shughuli zake za utoaji misaada ya kibinadamu unapaswa kutathmini kwa kina hali ya usalama nchini Nigeria.

Maiduguri, Nigeria

Msafara wa misaada ya kibinadamu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukitoka katika jimbo la  Borno ulishambuliwa hivi karibuni ukiwa njiani kuelekea Maiduguri.

Kusimamishwa shughuli hizo za utoaji misaada ni pigo kubwa hasa kwa kuzingatia kwamba, maafa ya wakimbizi wa Nigeria kutokana na njaa kali kaskazini mwa nchi hiyo, yamewatia wasi wasi wanaharakati wa haki za binaadamu.

wanachama wa Boko Haram

Mwanzoni mwa mwaka huu, Benki ya Dunia ilitangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram la nchini Nigeria hadi sasa wameua watu zaidi ya 20 elfu na kusababisha hasara ya dola bilioni 5.9 katika jimbo la Borno. Aidha ripoti hiyo ilisema zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa kundi hilo la Boko Haram.

Licha ya serikali ya Nigeria kutangaza kuwa imebadilisha mbinu za kupambana na Boko Haram, lakini inaonekana kuwa, kukabiliana na wanamgambo hao bado ni changamoto kubwa inayoikabili serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo.