Afrika Kusini: Hatutakubali kuburuzwa na Marekani
(last modified Fri, 07 Feb 2025 07:55:51 GMT )
Feb 07, 2025 07:55 UTC
  • Afrika Kusini: Hatutakubali kuburuzwa na Marekani

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa, taifa hilo halitakubali kuburuzwa na kushinikizwa na maajinabi.

Hii ni baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza mipango ya kuikatia misaada Afrika Kusini kutokana na eti sera zake za unyakuzi wa ardhi. Ramaphosa amesema nchi hiyo itajikita katika kuifanyia mageuzi mifumo yake ili kuimarisha uchumi na kukomesha utegemezi.

Jumatatu iliyopita pia, Ramaphosa alipinga bwabwaja za Trump na kusema kuwa, Pretoria haijawahi kunyakua ardhi yoyote ile. Alisema Afrika Kusini ni nchi huru na yenye demokrasia, na mambo yake ya ndani hayapaswi kuingiliwa na dola lolote lile, na kwa kisingizio chochote kile.

Wakati huo huo, Pretoria imesema haitaburuzwa na Washington baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio kutangaza kuwa atasusia mkutano ujao wa G20 mjini Johannesburg. Saa chache baada ya tangazo la Rubio jana Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Ronald Lamola alisisitiza tena msimamo huru wa nchi hiyo kuhusu masuala ya kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Ronald Lamola

Lamola amesema, "Sisi ni nchi huru na ya kidemokrasia iliyojitolea kwa utu, usawa na haki za binadamu, tukipigania kutobagua rangi na kutobagua jinsia huku tukiweka katiba yetu na utawala wa sheria mbele."

"Urais wetu wa G20 hauishii tu katika mabadiliko ya hali ya hewa lakini pia matibabu ya usawa kwa mataifa ya Kusini mwa Dunia, kuhakikisha mfumo sawa wa kimataifa kwa wote," mwanadiplomasia mkuu wa Afrika Kusini alisisitiza.

Rubio alitangaza kwamba hatashiriki mkutano wa kilele wa G-20 nchini Afrika Kusini uliopangwa kufanyika Februari 20-21, akidai kuwa taifa hilo mwenyeji linatekeleza "ajenda iliyo dhidi ya Marekani".