UN yaafiki kutumwa askari polisi nchini Burundi
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha pendekezo la Ufaransa la kutumwa askari polisi zaidi ya 200 wa umoja huo nchini Burundi kwa lengo la kuhitimisha machafuko ya zaidi ya mwaka mmoja nchini humo.
Katika kikao cha jana Ijumaa, baraza hilo liliafiki kutumwa maafisa wa polisi 228 katika mji wa Bujumbura na miji mingine nchini Burundi kwa muda wa mwaka mmoja. Nchi 11 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zilipiga kura ya kuunga mkono azimio hilo lililoandaliwa na Ufaransa, huku nchi nne za China, Misri, Angola na Venezuela zikijizuia kupigia kura. Polisi hao wa Umoja wa Mataifa watakuwa na jukumu la kulinda usalama sambamba na kusimamia haki za binaadamu kwa ushirikiano na waangalizi wa kimataifa na wataalamu wa masuala ya kijeshi wa Umoja wa Afrika nchini humo.
Awali serikali ya Bujumbura ilikubali pendekezo la Umoja wa Afrika la kutumwa askari 50 tu wa UN pamoja na waangalizi 100 wa umoja huo, na hatua hii ya Baraza la Usalama inatazamiwa kukosolewa na serikali ya nchi hiyo.
Itakumbwa kuwa, Burundi ilitumbukia kwenye mgogoro wa kisiasa kufuatia hatua ya chama tawala CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi uliopita, machafuko ambayo hadi sasa yamesababisha mauaji ya watu zaidi ya 500 huku wengine zaidi ya laki 2 na 70 elfu wakilazimika kuitoroka nchi na kuwa wakimbizi.