Warundi waandamana mbele ya ubalozi wa Ufaransa kupinga pendekezo lake UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12286-warundi_waandamana_mbele_ya_ubalozi_wa_ufaransa_kupinga_pendekezo_lake_un
Vyombo vya habari nchini Burundi vimearifu kuwa yamefanyika maandamano hadi mbele ya ubalozi wa Ufaransa mjini Bujumbura kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopendekezwa na serikali ya Paris.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 30, 2016 10:48 UTC
  • Warundi waandamana mbele ya ubalozi wa Ufaransa kupinga pendekezo lake UN

Vyombo vya habari nchini Burundi vimearifu kuwa yamefanyika maandamano hadi mbele ya ubalozi wa Ufaransa mjini Bujumbura kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopendekezwa na serikali ya Paris.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu Warundi wapatao 1000 wamefanya maandamano makubwa mbele ya ubalozi wa Ufaransa hii leo kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutaka kutumwa nchini Burundi askari 228, pendekezo ambalo awali lilitolewa na Paris. Vyombo vya habari vimeeleza kuwa, maandamano hayo yalianzia katika medani ya uhuru katikati ya jiji la Bujumbura kuelekea ubalozi wa Ufaransa ambapo waandamanaji walipiga nara dhidi ya Ufaransa na kutumwa askari hao wa Umoja wa Mataifa nchini humo.

Raia wa Burundi wakiwa katika maandamano mapema leo

Aidha waandamanaji wameituhumu Ufaransa kwamba, pendekezo hilo la kutumwa askari wenye silaha nchini Burundi ni njama za kutaka kutekeleza mauaji ya kimbari nchini humo kama yale yaliyowahi kutokea nchini Rwanda mwaka 1994. Hii ni katika hali ambayo kwa mara kadhaa serikali ya Burundi imekuwa ikikataa pendekezo la kutumwa askari wa kigeni na kusema kuwa, utumaji askari hao utahesabiwa kuwa ni uvamizi dhidi yake.