Rais wa Sudan Kusini ataka utulivu baada ya askari 28 kuuawa
(last modified Sat, 08 Mar 2025 07:01:58 GMT )
Mar 08, 2025 07:01 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini ataka utulivu baada ya askari 28 kuuawa

Jenerali wa Jeshi la Sudan Kusini na makumi ya wanajeshi wameuawa baada ya helikopta ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa ikijaribu kuwahamisha askari hao kutoka mji wa kaskazini wa Nasir iliposhambuliwa na genge la wanamgambo.

Rais Salva Kiir Mayardit ametoa wito wa utulivu baada ya Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la Sudan Kusini, David Majur Dak na askari wengine 27 kuuawa katika shambulio hilo la wanamgambo wa Jeshi Jeupu (White Army) katika Kaunti ya Nasir.

Rubani wa helikopta hiyo ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio hilo la jana Ijumaa. 

Wanajeshi hao wa Sudan Kusini walikuwa wakihamishwa kutoka Nasir na helikopta mbili za Umoja wa Mataifa waliposhambuliwa.

White Army ni kundi la wanamgambo ambalo serikali ya Rais Salva Kiir inalihusisha na vikosi vitiifu kwa mpinzani wake na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar.

Rais Salva Kiir (kushoto) na hasimu wake wa kisiasa, Riek Machar

Haya yanajiri siku chache baada ya Vikosi vya Sudan Kusini kumkamata Waziri wa Mafuta na maafisa kadhaa wakuu wa kijeshi waitifaki wa Machar; huku wanajeshi wakiendelea kuizingira nyumba yake katika mji mkuu, Juba.

Hakuna sababu iliyotolewa ya kukamatwa kwa shakhsia hao; kamatakamata ambayo imekuja baada ya kundi lenye silaha linaloshirikiana na Machar kuteka kambi ya jeshi katika jimbo la Upper Nile, kaskazini mwa nchi hiyo.