AU yatiwa wasiwasi na uhasama, taharuki nchini Sudan Kusini
(last modified Sun, 09 Mar 2025 11:24:28 GMT )
Mar 09, 2025 11:24 UTC
  • AU yatiwa wasiwasi na uhasama, taharuki nchini Sudan Kusini

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Moussa Faki Mahamat ametoa wito wa kusitishwa mara moja uhasama na mvutano wa kisiasa nchini Sudan Kusini.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi jioni, Mkuu huyo wa Umoja wa Afrika anayeondoka ameonyesha "wasiwasi mkubwa" juu ya mvutano unaoendelea katika Kaunti ya Nasir katika Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini. Mapigano hayo yanajumuisha shambulio baya dhidi ya helikopta ya Umoja wa Mataifa na ghasia za hapa na pale katika maeneo mengine, yote "yakitishia mchakato wa amani."

Huku akihimiza mamlaka husika kuwawajibisha kikamilifu waliohusika, Mahamat ametoa wito kwa pande zote kujizuia, kukomesha uhasama mara moja, kuzingatia mipango ya kusitisha mapigano na kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa.

Amesema AU kwa sasa inashauriana na mamlaka za Sudan Kusini, Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, Jumuiya ya Kiserikali ya Maendeleo ya Afrika Mashariki IGAD na washikadau wengine ili kuratibu juhudi za kupunguza mzozo huo.

Kabla ya hapo, Rais Salva Kiir Mayardit alitoa wito wa utulivu baada ya Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la Sudan Kusini, David Majur Dak na askari wengine 27 kuuawa katika shambulio la wanamgambo wa Jeshi Jeupe (White Army) katika Kaunti ya Nasir. White Army ni kundi la wanamgambo ambalo serikali ya Rais Salva Kiir inalihusisha na vikosi vitiifu kwa mpinzani wake na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar.

Helikopta ya Umoja wa Mataifa

Rubani wa helikopta hiyo ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio hilo la juzi Ijumaa. Wanajeshi hao wa Sudan Kusini walikuwa wakihamishwa kutoka Nasir na helikopta mbili za Umoja wa Mataifa waliposhambuliwa.

Haya yanajiri siku chache baada ya Vikosi vya Sudan Kusini kumkamata Waziri wa Mafuta na maafisa kadhaa wakuu wa kijeshi waitifaki wa Machar; huku wanajeshi wakiendelea kuizingira nyumba yake katika mji mkuu, Juba.