Rais wa Sudan Kusini awafuta kazi mawaziri 3
(last modified Tue, 11 Mar 2025 06:59:39 GMT )
Mar 11, 2025 06:59 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini awafuta kazi mawaziri 3

Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini amewafuta kazi mawaziri watatu jana Jumatatu katika mabadiliko yake ya hivi karibuni ndani ya Baraza la Mawaziri.

Katika uteuzi wa kwanza uliosomwa na Shirika la Utangazaji la Sudan Kusini (SSBC) linalomilikiwa na serikali, Rais Kiir amemfuta kazi Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba, Ruben Madol Arol na kumteuwa Wek Mamer Kuol achukue nafasi yake.

Katika uteuzi wake mwingine, Rais wa Sudan Kusini amemfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Elimu Awut Deng Acuil na kumteuwa Kuyok Abol Kuyok, na akamteuwa pia Atong Kuol Manyang kuwa Waziri wa Biashara na Viwanda na kuamuachisha kazi Joseph Mum Majak.

Taifa hilo lenye utajiri  wa mafuta lilijitenga na Sudan mwaka 2011, hata hivyo liliathiriwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya Rais Salva Kiir kuhitilafiana na Makamu wake Riek Machar.

Sudan Kusini inaendelea kushuhudia matukio mbalimbali ambapo siku kadhaa zilizopita Rais wa nchi hiyo Salva Kiir Mayardit alitoa wito wa kuwepo utulivu baada ya Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo David Majur Dak na askari wengine 27 kuuawa katika shambulio la wanamgambo wa Jeshi Jeupu (White Army) katika Kaunti ya Nasir.