UNHCR: Ghasia Sudan Kusini zimelazimisha watu 10,000 kukimbilia Ethiopia
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema ghasia katika kaunti za kaskazini mwa Sudan za Nasir na Ulang zimeongezeka kwa kasi, na kuwalazimu zaidi ya watu 10,000 kukimbilia nchi jirani ya Ethiopia.
Kufikia Jumatatu, zaidi ya watu 10,000 walikuwa wamevuka katika Mkoa wa Gambella nchini Ethiopia, kutoka 6,900 Machi 6, UNHCR imesema katika taarifa.
Shirika hilo la UN limesema, "Idadi inaongezeka kwa kasi ya kutisha na mamlaka za mitaa zinafuatilia na kusaidia watu waliofurushwa, kwani wametawanyika katika vijiji mbalimbali, hasa katika maeneo ya Burbiey na Matar."
Mapigano huko Nasir, mji wa kimkakati, yalishtadi baada ya Machi 3, na kusababisha kukamatwa kwa maafisa wakuu wa serikali na askari wa Sudan People's Liberation Movement/Army-In Opposition (SPLM/A-IO), linaloongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar. Zaidi ya watu 20 wameripotiwa kuuawa, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa viungani mwa mji wa Nasir, karibu na mpaka wa Sudan Kusini na Ethiopia.
Mnamo Machi 7, jenerali mmoja na makumi ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Sudan Kusini pamoja na mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa, waliuawa wakati askari wa Jeshi Jeupe (White Army), wanamgambo wanaoshirikiana na upinzani, waliwafyatulia risasi walipokuwa wakipanda helikopta ya Umoja wa Mataifa wakijaribu kuwahamisha huko Nasir.
(SPLM/A-IO) inayoongozwa na Riek Machar, imezihimiza Jumuiya ya IGAD na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC kuingilia kati na kusaidia kuachiliwa huru maafisa kadhaa wa upinzani wanaoshikiliwa na serikai ya Sudan Kusini.