Rais wa Gabon awatahadharisha wapinzani wake
Rais wa Gabon amewatahasharisha wapinzani wa serikali yake kuhusu kuzusha machafuko wakati wa uchaguzi.
Rais Ali Bongo Ondimba wa Gabon Jumapili hii ametahadharisha kuwa siasa zinazotekelezwa na wapinzani wa serikali yake kuhusu uchaguzi mkuu; ambao walihoji kuhusu ustahiki wake wa kuwa mgombea katika uchaguzi wa tarehe 27 mwezi Agosti, zinaweza kuibua machafuko nchini humo.
Ali Bongo Ondimba ameongeza kuwa hatua ya makundi mbalimbali ya upinzani kutangaza kuwa uchaguzi wa Rais wa Gabon hautakuwa wa wazi na huru, ni katika jitihada za kuzitia hofu na wasiwasi fikra za waliowengi. Rais wa Gabon amekanusha pia baadhi ya taarifa kwamba yeye ana asili ya Nigeria. Baadhi ya mahasimu wa Rais Ali Bongo wanaamini kuwa rais huyo hastahiki kugombea kiti cha rais kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo kutokana na kuwa si mzawa wa Gabon na kwamba ni mtoto aliyeasiliwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ina jukumu la kusimamia uchaguzi wa kisiasa nchini tayari imeidhinisha nyaraka na vithibitisho vya shakhsia 14 watakaogombea kiti cha urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 27 Agosti mwaka huu.