Jeshi la Sudan: Raia wasiopungua 41 wameuawa katika mashambulizi ya RSF huko al Fasher
Jeshi la Sudan leo Jumanne limetangza kuwa raia wengine wasiopungua 41 wameuawa na makumi ya wenegine kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora ya wanamgambo wa RSF katika mji wa al Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur ya Kaskazini, magharibi mwa Sudan.
Taarifa ya jeshi la Sudan imeeleza kuwa, wanawake na watoto ni miongoni mwa wahanga wa hujuma hiyo ya wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) iliyozilenga nyumba za makazi ya raia.
Jeshi la Sudan limeripoti kuwa vikosi vyake vimefanikiwa kujibu shambulio la RSF katika mji wa al Fasher na kuuwa wanamgambo 600 na kuharibu magari ya deraya 25 ya kikosi hicho.
Kikosi cha RSF hakijatoa tamko lolote kuhusu taarifa hii ya jeshi la Sudan.
Mapigano yanaendelea kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF huko al-Fasher tangu jana Jumatatu, suala ambalo limepelekea kusitishwa usambazaji wa chakula kwa raia walioathiriwa na vita.
Mji wa al-Fasher umekumbwa na mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF tangu Mei 2024, licha ya maonyo ya kimataifa kuhusu hatari ya mapigano katika mji huo, ambao unatumika kama kitovu cha operesheni za kibinadamu katika majimbo yote matano ya Darfur.
Mapema mwezi huu, wanamgambo wa kikosi cha RSF walida kuitwaa kambi ya wakimbizi ya Zamzam mjini humo baada ya makabiliano na vikosi vya jeshi. Takriban raia 400 waliuawa, na karibu 400,000 walikimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo.