Ripoti ya Umoja wa Mataifa: 84,000 wameathiriwa wa mafuriko Somalia
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana Jumanne imefichua kuwa zaidi ya watu 84,000 nchini Somaliawameathiriwa na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 17 tangu katikati ya mwezi uliopita.
Katika ripoti iliyochapishwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), wataalamu wa hali ya hewa wameonya juu ya uwezekano wa kunyesha mvua zaidi katika siku zijazo kusini na katikati mwa Somalia.
Eneo la Pembe ya Afrika ndilo eneo lililo hatarini zaidi kwa mabadiliko ya hali ya hewa, huku masafa na ukubwa wa matukio ya hali ya hewa yakiongezeka kwa kasi.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kuwa mafuriko ya ghafla yaliyosababishwa na mvua kubwa ya msimu yameua watu 17 na kuathiri zaidi ya wengine 84,000 katika maeneo kadhaa tangu katikati ya Aprili.
Mafuriko haya yanakuja wakati mashirika yasiyo ya kiserikali ya kutoa misaada yanakabiliwa na uhaba wa fedha ambao unatatiza uwezo wao wa kukabiliana na mahitaji ya dharura.
Somalia ilikumbwa na mafuriko makubwa mwaka 2023, ambayo yaliua zaidi ya watu 100 na wengine milioni moja wakalazimika kuyahama makazi yao, kutokana na mvua kubwa iliyosababishwa na hali ya hewa ya El Niño.