Uzinduzi wa chama kipya cha Gachagua wavurugwa na walioitwa "wahuni", Kenya
(last modified Thu, 15 May 2025 10:57:26 GMT )
May 15, 2025 10:57 UTC
  • Uzinduzi wa chama kipya cha Gachagua wavurugwa na walioitwa

Hafla ya uzinduzi wa chama kipya cha aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, cha Democracy for the Citizens Party (DCP) zimevurugwa mapema leo Alkhamisi baada ya kuingiliwa na watu waliotajwa na vyombo vya habari nchini humo kuwa ni "wahuni".

Tukio hilo limetokea asubuhi ya leo Alhamisi, muda mfupi baada ya msafara wa Gachagua kuondoka katika ukumbi wa hafla hiyo akiwa na maafisa wengine wakuu wa chama kipya cha DCP.

Hata hivyo, maafisa wa usalama walichukua hatua ya haraka na kuzima ghasia huku wahuni waliokamatwa na wafuasi wa Gachagua wakipigwa hadharani.

Maafisa usalama wa Kenya walifyatua risasi hewani wakati wa tukio hilo.

Nembo ya chama kipya ni sikio linalosikiliza, na kauli mbiu yake ni ‘Skiza Wakenya’, ikiwa na rangi za kijani kibichi yenye mwangaza, nyekundu ya kutu, na nyeupe.

Bw Gachagua amejiteua mwenyewe kuwa kiongozi wa chama na amewatangaza kaimu maafisa watakaosimamia chama hicho kipya.

“Kama Kiongozi wa Chama cha Democracy for the Citizens Party, naahidi kwamba nitasikiliza watu wa Jamhuri ya Kenya na kutimiza matakwa yao,” amesema Bw Gachagua.

Uchambuzi wa majina yaliyotangazwa kuongoza chama hicho unaonyesha kuwa wengi wao ni wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi mkuu uliopita. Wengine ni watu wasiokuwa maarufu.

Rigathi Gachagua amedai kuwa chama chake ni suluhisho kwa matatizo mengi yanayowakumba Wakenya, yakiwemo “mzigo wa ushuru, huduma mbovu za umma, gharama ya juu ya maisha, huduma duni za afya, sera mbaya, uongozi mbovu, ukosefu wa usalama na uongo wa kudumu.

Gachagua, aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, alitimuliwa na Bunge la Seneti miezi kadhaa iliyopita kwa mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake, yakiwemo kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu Idara ya Mahakama.