DRC yatishia kuweka vikwazo vikali zaidi vya mauzo ya madini adimu ya cobalt
(last modified Fri, 16 May 2025 02:18:46 GMT )
May 16, 2025 02:18 UTC
  • DRC yatishia kuweka vikwazo vikali zaidi vya mauzo ya madini adimu ya cobalt

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema kuwa inaweza kuweka vikwazo vikali zaidi vya mauzo ya cobalt wakati marufuku yake ya miezi minne itakapomalizika.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC inachangia karibu robo tatu ya uzalishaji wa madini wa cobalt duniani, lakini tangu mwezi Februari mwaka huu, imepitisha sheria ya kusitishwa mauzo ya nje ya madini hayo kwa miezi minne.

Kinshasa imesema kuwa hii ni kwa ajili ya kukabiliana na kuuzwa kiholela madini hayo duniani na kusababisha kushuka bei yake kwa kiasi kikubwa. Madini hayo adimu hutumika kutengeneza betri za lithiamu kwa magari ya umeme na simu erevu.

Kinshasa ilikuwa na matumaini kwamba marufuku yake ya kuuza bidhaa nje ingeleta utulivu wa soko na kulinda maslahi ya wazalishaji na wawekezaji wa Kongo. Lakini juzi Jumatano, mkuu wa wakala wa serikali wa kudhibiti madini ya kimkakati wa DRC alisema kwamba bei bado haijapanda kwani shehena za madini hayo yaliyokuwa yameuzwa kwa bei ya kutupa bado haijaisha na makampuni hayajawa bado na shida ya kununua shehena mpya.

Patrick Luabeya amesema kuwa, uamuzi unaofuata wa serikali ya Kinshasa ni kuweka vizuizi vikali zaidi vya mauzo ya nje ya madini hayo ya cobalt ili kuleta mshituko katika soko lake na kufikisha bei kwenye kiwango kinachostahiki. 

Ameongeza kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Masoko ya Kimkakati ya Bidhaa za Madini itashauriana na wadau wa sekta hiyo mwezi ujao wa Juni kuhusu marufuku hiyo na hatua gani kali zaidi zinapaswa kuchuliwa.