Rais wa zamani wa Mauritania aongezewa kifungo, sasa ni miaka 15 jela
(last modified Fri, 16 May 2025 02:21:37 GMT )
May 16, 2025 02:21 UTC
  • Rais wa zamani wa Mauritania aongezewa kifungo, sasa ni miaka 15 jela

Mahakama ya rufaa ya Mauritania imemhukumu rais wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Ould Abdel Aziz kifungo cha miaka 15 jela kwa tuhuma za ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka na utakatishaji fedha.

Abdel Aziz, ambaye aliongoza Mauritania kuanzia Agosti 5, 2009 hadi Agosti 1, 2019, awali alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kabla ya kukata rufaa.

Wakili wake, Mohameden Ould Ichidou, amesema kuwa mteja wake ana nia ya kuwasilisha rufaa mbele ya Mahakama ya Juu, akisema kwamba uamuzi wa mahakama hiyo dhidi yake umechangiwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Kwa upande wake, Ibrahim Ould Ebety, wakili wa chama cha kiraia kinachowakilisha serikali, amesifu hukumu hiyo na kusema kwamba ushahidi uliowasilishwa mahakamani ni madhubuti uliotiwa nguvu na ukweli usiokanushika.

Mwezi Januari 2023 polisi nchini Mauritania walimtia mbaroni rais huyo wa zamani wa nchi hiyo Mohamed Ould Abdelaziz kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kujilimbikizia mali kinyume cha sheria. 

Mohamed Ould Abdelaziz aliye na umri wa miaka 68 awali alitakiwa kuripoti kituo cha polisi lakini alikataa. Mawakili wanaomtetea walieleza kuwa, mwezi Januari 2023, polisi walifika nyumbani kwa rais huyo wa zamani wa Mauritania katika mji mkuu Nouakchott wakiwa na waranti wa kumtia nguvuni na kisha walimkamata. 

Jenerali huyo mstaafu aliingia madarakani nchini Mauritania kupitia mapinduzi ya kijeshi na alibakia madaraka kwa muda wa miaka 11. Mohamed Ould Abdelaziz alijizulu mwaka 2019 baada ya kumalizika mihula yake miwili ya urais.