Misri yarejesha nyumbani mabaki 21 ya kale yaliyoibwa na kupelekwa Australia
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza kwamba, nchi hiyo imefanikiwa kurejesha nyumba, mabaki 21 yenye thamani kubwa ya mabaki ya kali yaliyokuwa yameibwa nchini humo na kupelekwa Australia.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema: Kwa kushirikiana na mamlaka huzika za Australia, maafisa wa kibalozi wa Misri huko Canberra na Sydney wamefanikiwa kurejesha nyumbani mabaki 21 yenye thamani kubwa ya kale yalilyopatikana yakioneshwa kinyume cha sheria kwenye nyumba moja ya mnada nchini Australia.
Taarifa hiyo pia imesema: "Kurejeshwa mabaki hayo kumekwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 75 ya uhusiano wa kidiplomasia wa Misri na Australia. Hatua hiyo imechukuliwa ili kuonesha kwamba ushirikiano wa pande hizo mbili katika kulinda turathi za kitamaduni na kupambana na magendo ya mabaki ya kale ni mkubwa."
Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imebainisha pia kwamba nchi hiyo inafanya juhudi kubwa za kuhifadhi turathi zake, huku wizara hiyo ikichukua jukumu kubwa katika kurejesha Misri bidhaa zilizotoroshwa kimagendo kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale na Baraza Kuu la Mambo ya Kale.
Misri imezidisha kampeni yake ya kimataifa katika miaka ya hivi karibuni ya kurejesha vitu vya kale vilivyoibwa na kupelekwa kimagendo nje ya nchi. Siku ya Jumatatu, Misri ilitangaza kurejesha vitu 25 muhimu vya kihistoria na kisanii, vinavyohusiana na vipindi vingi vya ustaarabu wa kale wa Misri, kutoka nchini Marekani.