Ufaransa yafuta uchunguzi wa uhalifu dhidi ya mjane wa Rais wa zamani wa Rwanda
(last modified Fri, 23 May 2025 02:58:34 GMT )
May 23, 2025 02:58 UTC
  • Ufaransa yafuta uchunguzi wa uhalifu dhidi ya mjane wa Rais wa zamani wa Rwanda

Ufaransa imetangaza kuwa, imefuta uchunguzi wa uhalifu dhidi ya mjane wa Rais wa zamani wa Rwanda

Mahakama ya rufaa ya Ufaransa imeamua kwamba uchunguzi dhidi ya Agathe Kanziga Habyarimana, Mke wa Rais wa zamani wa Rwanda, hautaendelea.

Agathe Habyarimana, 82, ambaye amekuwa akiishi Ufaransa tangu 1998 na ambaye kurejeshwa kwake Rwanda kumeombwa mara kwa mara na Kigali, hatakabiliwa na ufuatiliaji wa mahakama ya Ufaransa katika hatua hii, duru zimesema, zikiomba kutotajwa.

Uamuzi huo unafuatia hitimisho la jaji wa uchunguzi kwamba "hakuna ushahidi wa kutosha" wa kumfungulia mashtaka mjane wa Rais wa zamani Juvenal Habyarimana mwenye umri wa miaka 82 kwa madai ya kuhusika katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi, yaliyoanza Aprili 7, 1994.

Uamuzi wa mahakama hiyo unahusu rufaa iliyowasilishwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Kitaifa wa Ufaransa wa Kupambana na Ugaidi, ambayo ilikuwa imeomba uchunguzi uendelee kuwa wazi.

Upande wa mashtaka pia uliiomba mahakama kupanua wigo wa kesi hiyo ili kujumuisha mashtaka yanayoweza kutokea ya njama ya kufanya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu na kuongeza muda wa uhalifu kujumuisha kipindi cha kabla ya mauaji ya kimbari, kuanzia Machi 1, 1994.

Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalitokea kwa muda wa siku 100 kuanzia Aprili 6 mwaka 1994 baada ya Rais Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote Wahutu, kupoteza maisha wakati ndege yao ilipotunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.