AU haiwezi kufurahishwa na njama za kuwapora Wapalestina na kuwapeleka barani Afrika
(last modified Fri, 23 May 2025 06:25:51 GMT )
May 23, 2025 06:25 UTC
  • AU haiwezi kufurahishwa na njama za kuwapora Wapalestina na kuwapeleka barani Afrika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola Tete Antonio amesema kuwa, Umoja wa Afrika (AU) hauwezi kuwa na furaha unapoona kuna njama za kuwapora Wapalestina ardhi zao na kuwapeleka barani Afrika.

Antonio amesema hayo mbele ya waandishi wa habari akiwa pamoja na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, na baada ya kumalizika mkutano wa tatu wa mawaziri wa EU-AU mjini Brussels.

Amesema: "Kwa hakika tunatetea suluhisho la serikali mbili, mataifa mawili bega kwa bega na kuheshimiwa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.”

Akiuwakilisha Umoja wa Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola pia amesema: “Msimamo wa AU wa kuwaunga mkono Wapalestina na watu wanaodhulumiwa utaendelea kuwa vilevile.”

Amesema: Mgeni pekee mwalikwa wa kudumu wa AU katika mikutano yake ya kilele alikuwa ni Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, akiongeza kuwa jambo hilo linaonesha msimamo wa AU kuhusu Palestina.

Kwa upande wake, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya amesisitizia uungaji mkono umoja huo kwa AU katika juhudi zake za upatanishi wa kikanda na kusema: "Michakato yote hiy ya barani Afrika inapaswa kuongozwa na Waafrika na kumilikiwa na Waafrika wenyewe, hata kama upatanishi unahitajika."

Kallas pia amesema hivi sasa kuna vita vya upashaji habari kila mahali, na habari potofu ni moja ya zana ambazo zinatumiwa hasa kuhusu bara la Afrika.

"Tunapaswa kupambana na habari potofu na ushawishi mbaya wa kigeni wakati wote," aliongeza.