Sudan Kusini yakubali kutumwa askari wa kieneo nchini
Serikali ya Sudan Kusini imekubali pendekezo la jumuiya ya kieneo ya IGAD la kutumwa askari wa kulinda amani nchini humo, suala ambalo awali lilikuwa limepingwa vikali na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo.
Mahboub Maalim, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD amesema hayo baada ya mkutano wa dharura wa wakuu wa jumuiya hiyo hapo jana mjini Addis Ababa nchini Ethiopia na kuongeza kuwa, Taban Deng Gai amekubali kujiuzulu wadhifa wake wa Makamu wa Kwanza wa Rais mara tu Riek Machar atakaporejea mjini humo.

Kufuatia mapigano kati ya askari wa serikali na upinzani yaliyosababisha mauaji ya watu wasiopungua 300, Rais Salva Kiir alimteua Taban Deng Gai kuwa makamu wake baada ya Machar kuutoroka mji wa Juba na kuapa kutorejea hadi askari wa kieneo wa kulinda amani watumwe nchini humo. Hata hivyo Samuel Makuei, Waziri wa Habari wa Sudan Kusini alikanusha taarifa kuwa Rais Salva Kiir ndiye aliyemteua Taban Deng Gai kujaza nafasi ya Riek Machar na kusisitiza kuwa, uteuzi huo ulifanywa na chama chenyewe cha upinzani cha SPLM.

Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Salva Kiir kuwapiga kalamu nyekundu mawaziri sita wa upande wa makamu wake wa zamani yaani Riek Machar.
Mapigano hayo yanafanyika licha ya uwepo wa askari 12,000 wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa UNMISS katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.