11 wauawa Kenya katika maandamano ya kumbukumbu ya vuguvugu la demokrasia
Watu wasiopungua 11 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka 35 ya kumbukumbu ya vuguvugu la kupigania demokrasia maarufu kama Saba Saba.
Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya imesema, imebaini matukio mawili ya utekaji pamoja na watu 37 kukamatwa katika kaunti 17.
Aidha kumekuwepo na matukio ya uporaji katika kaunti sita, na ofisi moja ya kuratibu masuala ya eneo bunge katika mkoa wa kati ilichomwa moto na wanaoshukiwa kuwa wahalifu.
Taarifa ya polisi imesema, askari 52 wamejeruhiwa pia katika makabiliano na waandamanaji.
Maandamano hayo ya Saba Saba ya jana Jumatatu yaliyoshirikisha maelfu ya watu yalikuwa ya kuadhimisha mapambano ya kudai demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya ya Julai 7, 1990, lakini yalichanganyika pia na miito ya kumtaka Rais William Ruto ajiuzulu.
Yakiwa yamechochewa na ugumu wa maisha, ukatili wa polisi, na msururu wa mauaji ya watu wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, maandamano hayo yaliratibiwa na tabaka la vijana wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya haki za binadamu huenda idadi ya waliouawa ikaongezeka.../