Upinzani Uganda wafungua kesi mahakamani kupinga raia kushtakiwa kwenye mahakama ya kijeshi
Chama kikuu cha upinzani nchini Uganda cha Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (National Unity Platform) NUP, kimefungua kesi katika Mahakama ya Katiba ya kutaka sheria mpya iliyorudisha haki ya mahakama za kijeshi kusikiliza kesi za raia ifutwe.
Wakili wa NUP, George Musisi, amesema chama hicho kimewasilisha ombi la kufutwa sheria mpya ambayo bunge liliipitisha mwezi Mei na Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni akaisaini mwezi mmoja baadaye.
Baada ya Museveni, mwenye umri wa miaka 80, kusaini sheria hiyo, msemaji wa jeshi wa wakati huo, Chris Magezi, aliisifu akisema itazuia kuundwa kwa makundi ya kisiasa yenye misimamo mikali, huku mkuu wa jeshi la Uganda, Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais Museveni, akiwapongeza wabunge kwa kupitisha sheria hiyo.
Katibu Mkuu wa NUP Lewis Rubongoya, ametilia mkazo dai la chama chake kwa kusema: "walikiuka taratibu zote ambazo walipaswa kufuata wakati wa kupitisha sheria," na akaashiria kutoshirikishwa umma katika suala hilo.
Mnamo mwezi Januari, Mahakama ya Juu ya Uganda ilipiga marufuku kuwahukumu raia katika mahakama za kijeshi ikisema mahakama hizo hazina uwezo wa kisheria wa kuendesha kesi za jinai kwa njia ya haki na isiyo na upendeleo.
Wafuasi wengi na viongozi wa NUP, akiwemo mwanasiasa machachari Bobi Wine ambaye anajiandaa kumkabili Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi wa mwaka ujao, hapo awali walishitakiwa au kuhukumiwa na mahakama za kijeshi.../