Je, ushirikiano wa kijeshi wa Marekani na Nigeria unaongeza hatari ya ukiukaji wa haki za binadamu?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129962-je_ushirikiano_wa_kijeshi_wa_marekani_na_nigeria_unaongeza_hatari_ya_ukiukaji_wa_haki_za_binadamu
Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuwa ili kuisaidia Nigeria katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi, imekubali kuiuzia nchi hiyo silaha zenye thamani ya takriban dola milioni 346.
(last modified 2025-08-25T05:53:34+00:00 )
Aug 25, 2025 05:53 UTC
  • Je, ushirikiano wa kijeshi wa Marekani na Nigeria unaongeza hatari ya ukiukaji wa haki za binadamu?

Hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuwa ili kuisaidia Nigeria katika mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi, imekubali kuiuzia nchi hiyo silaha zenye thamani ya takriban dola milioni 346.

Silaha hizo ni pamoja na risasi, mabomu na maroketi yanayoongozwa kutokea mbali, ambazo Washington inadai zinatumwa Nigeria kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya vitisho vya ugaidi kama vile Boko Haram na Daesh barani Afrika.

Lakini uamuzi huu, ambao kinadhihiri unaonekana kulenga kuimarisha usalama wa kieneo, umezua wimbi la wasiwasi miongoni mwa wananchi wa Nigeria na hata baadhi ya maafisa wa nchi hiyo na vile vile Marekani. Wasiwasi huu unatokana na ukweli kwamba licha ya madai ya kusaidia kupambana na ugaidi, utoaji wa silaha hizi unaweza kuongeza migogoro ya ndani na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Nigeria.

Katika miaka ya hivi karibuni, Nigeria imekabiliwa na changamoto kubwa katika uwanja wa usalama na utulivu wa kisiasa. Kwa upande mmoja, makundi yenye misimamo mikali kama vile Boko Haram, Daesh na wanamgambo wengine yanaendesha harakati zao katika maeneo ya kaskazini na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na hivyo kuchochea ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. Kwa upande wa pili, katika maeneo ya kusini na katikati mwa Nigeria, machafuko na maandamano ya kijamii yanayosababishwa na vitendo vya kuenea rushwa, ukosefu wa ajira na fursa za kiuchumi yameenea ambapo vikosi vya usalama vya Nigeria pia vinashutumiwa kwa kukiuka haki za binadamu na kukandamiza upinzani wa ndani, haswa kuhusiana na migogoro ya kijamii na kiuchumi.

Vikosi vya Jeshi la Nigeria, haswa jeshi na polisi, vimekuwa vikituhumiwa mara kwa mara kwa ukiukaji wa haki za binadamu katika miaka ya hivi karibuni. Kuna ripoti kadhaa zinazoonyesha kwamba vikosi hivyo vinatumia silaha za kigeni kukandamiza maandamano na kushambulia makundi ya kikabila na kidini, ambapo katika baadhi ya matukio, ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu umeripotiwa. 

Hali hii imeibua wasiwasi kuhusu matumizi mabaya ya silaha za kigeni na athari zake mbaya kwa haki za binadamu nchini Nigeria.

Maandamano Nigeria

Hata hivyo, Washington inaendelea kudai kwamba inaisaidia nchi hiyo kupambana na ugaidi.

Kwa mtazamo mwingine, uuzaji wa silaha kwa Nigeria unaweza kuchukuliwa kuwa ni mwendelezo wa siasa za Marekani za kupanua uhusiano wa kisiasa na kijeshi na nchi hiyo yenye ushawishi mkubwa katika eneo la Afrika Magharibi.

Kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikijaribu kupanua uwepo wake katika maeneo tofauti ya Afrika, na sasa upanuzi wa uhusiano wa kijeshi na Nigeria, kama nguvu kubwa ya kijeshi katika eneo hilo, ni muhimu sana kwa nchi zote mbili. Ni wazi kuwa, kuimarishwa nguvu ya kijeshi ya Nigeria kunaweza kudumisha na kuzidisha ubora wa kijeshi wa nchi hii katika eneo hilo.

Kwa hakika nchi za Magharibi hususan katika miaka ya hivi karibuni zimekabiliwa na vikwazo vikubwa na maandamano ya kisiasa na kijamii kutokana na mwamko wa kisiasa wa nchi nyingi za Afrika. Kwa kadiri kwamba viongozi wa Marekani wamelazimika kufunga vituo vyao vya kijeshi katika nchi nyingi za Afrika, ikiwa ni pamoja na Niger. Kwa hivyo, madai ya kusaidia kupambana na ugaidi hivi sasa ni fursa muhimu  kwa viongozi wa Washington kwa mara nyingine tena kupanua uhusiano wao wa kijeshi na kisiasa na nchi za bara la Afrika. Ikiwa mikataba ya aina hiyo itatiwa saini, kuna uwezekano pia wa kuimarishwa mahusiano ya kiuchumi ya pande mbili. Hasa kwa vile Nigeria ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta na mshirika wa kibiashara wa Marekani katika uwanja huu.

Kwa vyovyote vile hata kama uuzaji wa silaha kwa Nigeria unaonyeshwa kidhahiri kuwa hatua ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugaidi, lakini maslahi ya kisiasa, kijamii na kibinadamu ya suala hilo hayapaswi kupuuzwa. Katika muktadha huo, kuna wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa kutumiwa vibaya silaha hizo na kuongezeka migogoro ya ndani katika nchi hiyo ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa ya kiusalama na ukiukaji wa haki za binadamu. Pia kuna wasiwasi mwingi kuhusu kuimarishwa uwepo wa Marekani nchini Nigeria na kuongezeka mashinikizo ya kisiasa na kijeshi dhidi ya nchi hii ya Kiafrika ili iendane na siasa za Washington.