Somalia kuelekea kwenye siasa za vyama ili kuondoa ushindani wa kikoo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13024-somalia_kuelekea_kwenye_siasa_za_vyama_ili_kuondoa_ushindani_wa_kikoo
Kongamano la viongozi wa kanda na wa kitaifa wa Somalia limetangaza kuwa wabunge watakaochaguliwa katika bunge jipya litakaloundwa mwaka huu watalazimika kujiunga na chama cha siasa ndani ya kipindi cha miaka miwili au kujiuzulu, ikiwa ni katika juhudi za kuliondoa taifa hilo la Pembe ya Afrika kwenye siasa za kikoo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 11, 2016 00:02 UTC
  • Ramani ya Somalia
    Ramani ya Somalia

Kongamano la viongozi wa kanda na wa kitaifa wa Somalia limetangaza kuwa wabunge watakaochaguliwa katika bunge jipya litakaloundwa mwaka huu watalazimika kujiunga na chama cha siasa ndani ya kipindi cha miaka miwili au kujiuzulu, ikiwa ni katika juhudi za kuliondoa taifa hilo la Pembe ya Afrika kwenye siasa za kikoo.

Kongamano la Jukwa la Kitaifa la Uongozi lililofanyika kwa muda wa juma zima limetangaza kuwa washiriki wamekubaliana kushajiisha uanzishaji na usajili wa vyama vya siasa  ndani ya kipindi cha miaka miwili  bunge la 10 litakapochaguliwa.

Wabunge wa Sonalia wakila kiapo

Jukwaa hilo lililohudhuriwa pia na Rais Hassan Sheikh Mohamud, mawaziri na viongozi wa kanda  limetangaza kuwa vyama hivyo vya siasa vitapaswa kusajili wanachama na kwamba wabunge wote watatakiwa wawe wamejiunga na chama kimojawapo ifikapo Oktoba 20 mwaka 2018. Mbunge yeyote atakayeshindwa kujiunga na chama hadi wakati huo atapoteza kiti chake. 

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia

Japokuwa hivi sasa baadhi ya wabunge wanafanya kazi kama mrengo mmoja lakini hakuna muundo rasmi wa kichama au mfumo wa kusajili vyama nchini Somalia kwa sasa.

Somalia inapiga hatua za kujijenga upya kwa mwendo wa kujikongoja baada ya zaidi ya miongo miwili ya migogoro na machafuko ambayo kwa sehemu kubwa yamechangiwa na uhasama na ushindani wa kikoo. Nchi hiyo ya Pembe ya Afrika itafanya uchaguzi wa kuchagua bunge jipya mwezi ujao wa Septemba ambalo mwezi Oktoba litamchagua rais mpya wa nchi hiyo.../