Wakenya 66,000 kupoteza ajira ikiwa makubaliano ya AGOA hayatatazamwa upya
Sheria ya Ukuaji na Fursa Barani Afrika (AGOA) inatazamiwa kumalizika muda wake ifikapo tarehe 30 mwezi huu wa Septemba, na hivyo kuhitimisha mpango muhimu wa biashara bila ushuru kati ya Kenya na Marekani.
Mkataba huo unatajwa kuleta mageuzi makubwa, ukiimarisha mabilioni ya shilingi katika uwekezaji, ukiendeleza ajira zipatazo 66,000 katika sekta ya utengenezaji nguo na kusaidia karibu Wakenya 660,000 ambao wanategemea sekta ya mavazi kudhamini maisha yao. Bila AGOA, Kenya itapoteza kasi yake ya ushindani dhidi ya Bangladesh, Vietnam, na Misri.
Serikali ya Kenya imechukua hatua haraka na kuamua kumtuma mjini Washington Waziri wa Biashara, Lee Kinyanjui ili kuomba kuongezewa muda.
Kenya italazimika kutekeleza mabadiliko ya haraka iwapo sheria ya AGOA haitaongezwa muda. Mkataba wa Biashara Huria kati ya Kenya na Marekani (FTA) unaweza kutoa mwanya kwa wawekezaji kuhakikisha kuwa Kenya inashiriki katika misururu ya ugavi duniani.
Mbali na sekta ya utengenezaji mavazi, mustakabali wa Kenya unategemea pia uuzaji nje mazao ya kilimo kama karanga, kilimo cha bustani, na hata bidhaa zilizoongezwa thamani huku Marekani ikisalia soko kubwa zaidi la bidhaa hizo duniani.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, Kenya inaweza kuwa mfano wa mageuzi ya viwanda na kilimo iwapo hatua ya zilizoratibiwa zitachukuliwa katika kipindi hiki cha changamoto.