Mkutano wa pili wa hali ya hewa Afrika wazinduliwa Addis Ababa, Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130592-mkutano_wa_pili_wa_hali_ya_hewa_afrika_wazinduliwa_addis_ababa_ethiopia
Mkutano wa Pili wa Hali ya Hewa wa Afrika ulizinduliwa jana huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia huku viongozi wakitoa wito wa kuachana na utoaji matamshi pekee na kujikita katika uchukuaji hatua.
(last modified 2025-09-09T07:11:14+00:00 )
Sep 09, 2025 07:11 UTC
  • Mkutano wa pili wa hali ya hewa Afrika wazinduliwa Addis Ababa, Ethiopia

Mkutano wa Pili wa Hali ya Hewa wa Afrika ulizinduliwa jana huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia huku viongozi wakitoa wito wa kuachana na utoaji matamshi pekee na kujikita katika uchukuaji hatua.

Akifungua mkutano huo, Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa Ethiopia amezihimiza nchi washirika kuwekeza barani Afrika.

Waziri Mkuu wa Ethiopia ameashiria pia Mpango wa Ubunifu wa Kijani wa Ethiopia, wa kupanda miti zaidi ya bilioni 48 na kuanzishwa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance, mradi ambao unatazamiwa kuzalisha megawati 5,000 za nishati mbadala.

"Hatuko hapa kujadili maisha yetu. Tuko hapa kubuni uchumi ujao wa hali ya hewa duniani. Wakati ardhi ya Afrika inapona, mito na hali yetu ya hewa inapokuwa safi; bara la Afrika huwa limeshinda",amesema Waziri Mkuu wa Ethiopia.

Abiy Ahmed pia amependekeza Mkataba wa Ubunifu wa Hali ya Hewa wa Afrika, kutengwa dola bilioni 50 kwa mwaka ili kutatua changamoto za mabadiliko ya tabia nchi barani Afrika katika nyanja za nishati, kilimo, maji, usafiri na n.k hadi kufikia mwaka 2030.

Waziri Mkuu wa Ethiopia pia amewasilisha ombi rasmi kwa ajili ya nchi yake kuwa mweyeji wa Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi mwaka 2027.

Naye Mahmoud Ali Youssouf Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesisitiza katika Mkutano wa Pili wa Hali ya Hewa wa Afrika udharura wa kuwepo usawa katika ufadhili wa kimataifa. 

Amesema, Kamisheni ya Umoja wa Afrika inaamini kuwa fedha za ufadhili ya masuala ya hali ya hewa zinapasa kutolewa kwa uadilifu.

Mkutano huo wa siku tatu unajumuisha sherehe ya upandaji miti katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Addis Ababa, ambapo wakuu wa nchi waliahidi umoja na kujitolea kurejesha mifumo ikolojia.