Besigye amtaka Mkuu wa Polisi Uganda ajiuzulu
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Dakta Kizza Besigye amemtaka Mkuu wa Polisi nchini humo ajiuzulu mara moja, kufuatia kesi ya jinai inayomkabili.
Akihutubia waandishi wa habari nyumbani kwake Kasangati hii leo, Besigye amesema kama Kale Kayihura anaheshimu sheria za nchi, anapaswa ajiuzulu wadhifa wake. Kinara wa upinzani nchini Uganda ameongeza kuwa: "Mimi kama wakili namshauri Jenerali Kayihura ajiengue madarakani, kesi ya jinai dhidi yake itaamua mustakabali wa mfumo wa sheria nchini na ni vyema ajiuzulu ili kuepuka mgongano wa maslahi."
Matamshi ya Besigye yanajiri siku moja baada ya wafuasi wa Jenerali Kayihura kuandamana nje ya majengo ya mahakama mjini Kampala ambapo kesi dhidi ya mkuu huyo wa Polisi ilikuwa inasikilizwa.
Inspekta Jenerali wa Polisi wa Uganda pamoja na makamanda wengine 7 waandamamizi wa polisi ya nchi hiyo wanatuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya wafuasi wa Besigye, wakati na baada ya uchaguzi mkuu uliopita.
Itakumbukwa kuwa, watu 22 waliuawa katika mapigano yaliyojiri magharibi mwa nchi hiyo kati ya wafuasi wa Museveni na Besigye, baada ya uchaguzi wa Februari 18 mwaka huu. Chama cha upinzani cha FDC kiliituhumu serikali ya Uganda kuwa imechochea machafuko hayo na kwamba ilitumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na wafuasi wa upinzani.