Majaliwa: Rais Samia anatambua mchango wa madhehebu ya dini katika kuendeleza maarifa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua kwa dhati mchango wa madhehebu ya dini likiwemo Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) na wadau wote wa elimu katika kuimarisha maadili, kuendeleza maarifa na kuleta mshikamano wa kitaifa kupitia elimu.
Majaliwa maebainisha haya jana alipomwakilisha Rais Dkt. Samia katika hafla ya usiku ya utoaji tuzo za elimu za Mufti iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Serena hotel jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa elimu haiwezi kukamilika kama hakuna maadili kwani ndiyo yanayojenga utu, heshima na mshikamano wa kijamii. “Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha elimu inakuza maarifa na ujuzi, sambamba na malezi yanayoimarisha tabia bora na maadili ya kizalendo kwa vijana wa Kitanzania”.
“Rais Dkt. Samia anawapongeza sana BAKWATA kwa juhudi kubwa mnazozifanya katika masuala yote ya maendeleo ya jamii hususan mchango wenu katika kuendeleza elimu na kuimarisha mshikamano wa kitaifa kupitia malezi ya maadili na maarifa, Serikali inathamini sana mchango wa taasisi za dini kama BAKWATA katika kuunga mkono malezi ya watoto na vijana”. Alisema Mheshimiwa Majaliwa jana Jumamosi.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Tuzo za Elimu za Mufti ni jukwaa la kitaifa la kutambua na kuthamini michango ya kipekee katika elimu, ubunifu, malezi na maadili ya vijana wa Kitanzania. “Tukio hili linaakisi muonekano wa taifa lenye watu wanaojituma, wanaothamini elimu, na wanaochangia ustawi wa taifa letu bila kujali itikadi za dini au misimamo ya kisiasa.”