Feb 15, 2016 15:25 UTC
  • Zaidi ya watu 50 wafariki dunia kwa homa ya manjano nchini Angola

Mkuu wa idara ya taifa ya afya nchini Angola amesema kuwa, watu 51 wamefariki dunia katika kipindi cha chini ya miezi mwili katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kutokana na homa ya manjano.

Kwa mujibu wa afisa huyo mwandamizi wa afya nchini Angola, watu 240 wamekumbwa na homa ya manjano nchini humo na tayari 51 kati yao wameshapoteza maisha.

Amesema, zaidi ya watu 450 wameshapigwa chanjo ya kuzuia ugonjwa huo katika mji mkuu Luanda, ambacho ndicho kituo kikuu cha kuenea homa hiyo hatari nchini Angola.

Ugonjwa wa homa ya manjano umeenea nchini Angola katika hali ambayo nchi hiyo imekumbwa na nakisi kubwa ya bajeti kutokana na kuporomoka bei ya mafuta kiasi kwamba hata bajeti ya fedha za kukusanya takataka imefutwa na matokeo yake ni kurundikana taka katika maeneo ya watu maskini au kwenye vituo vya mabasi na kuandaa mazingira ya kuzaliana mbu wanaosambaza virusi vya ugonjwa huo.

Si hayo tu, lakini pia wafanyakazi wengi wa masuala ya afya na usafi nchini Angola wanalalamikia kutolipwa mishahara yao.

Kesi ya kwanza ya homa ya manjano iliripotiwa mwezi Disemba mwaka jana huko Angola, nchi ambayo asilimia 95 ya bajeti yake inategemea kuuza mafuta ghafi nje ya nchi.

Bei ya mafuta imepungua kwa asilimia 70 tangu katikati ya mwaka 2014 na kupelekea kuporomoka thamani ya sarafu ya nchi hiyo ambayo inahesabiwa kuwa ya tatu kwa kuwa na uchumi mzuri barani Afrika.

Tags