Wataalamu wa UN: Utesaji na ukatili wa kingono unaongezeka Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13150-wataalamu_wa_un_utesaji_na_ukatili_wa_kingono_unaongezeka_burundi
Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametangaza kuwa utesaji dhidi ya wakosoaji wa serikali wanaowekwa kizuizini nchini Burundi unaongezeka; na vikosi vya usalama vinafanya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake wakati wa maandamano ya upinzani na wanapofanya upekuzi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 12, 2016 22:22 UTC
  • Wataalamu wa UN: Utesaji na ukatili wa kingono unaongezeka Burundi

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametangaza kuwa utesaji dhidi ya wakosoaji wa serikali wanaowekwa kizuizini nchini Burundi unaongezeka; na vikosi vya usalama vinafanya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake wakati wa maandamano ya upinzani na wanapofanya upekuzi.

Kamati ya kupambana na utesaji ya Umoja wa Mataifa imeeleza wasiwasi ilionao kutokana na utoaji kauli za kuashiria chuki za kimbari unaofanywa na maafisa waandamizi wa serikali katika mgogoro unaoendelea kwa muda wa mwaka sasa katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.

Jens Modvig, mwenyekiti wa jopo la kamati hiyo wa wataalamu 10 wa haki za binadamu amewaeleza waandishi wa habari kwamba wana ripoti na taarifa zinazoonyesha kuwa ukatili na utesaji unachochewa na sababu za kisiasa.

Amesema utesaji huo unaolenga makundi fulani ya kisiasa na kimbari unaweza kuwa ishara ya onyo la mapema juu ya mwenendo unaoweza kuishia kwenye mauaji ya kimbari.

Jens Modvig, mwenyekiti wa jopo la wataalamu wa UN

Jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa limeitaka serikali ya Bujumbura iwe na udhibiti mkali kwa jeshi lake la Polisi na askari wa usalama na kukomesha jinai zikiwemo za watu kuuliwa bila ya kufikishwa kwenye vyombo vya mahakama, utesaji na utowekaji wa watu. Aidha wametaka uchunguzi ufanyike na wahusika washtakiwe.

 Baada ya kuchunguza rekodi za serikali, wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa vitendo vingi vya utesaji hufanywa katika idara ya taifa ya Intelijinsia iliyoko karibu na mji mkuu Bujumbura lakini pia kwenye vituo vya siri vya kuwekea watu kizuizini.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Watu zaidi ya 450 wameuliwa nchini Burundi tangu Rais Pierre Nkurunziza aliposhinda urais kwa muhula wa tatu huku wengine zaidi ya laki mbili wakilazimika kuihama nchi na kuwa wakimbizi katika nchi jirani. Wapinzani wake wanasema hatua yake ya kugombea urais ilikiuka katiba na makubaliano yaliyohatimisha vita vya ndani ya mwaka 2005.../