Maafisa usalama wa Somalia kupatiwa mafunzo zaidi na kikosi cha AMISOM
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13258-maafisa_usalama_wa_somalia_kupatiwa_mafunzo_zaidi_na_kikosi_cha_amisom
Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimeazimia kuongeza kozi za mafunzo kwa maafisa usalama wa nchi hiyo ya pembe ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 14, 2016 09:47 UTC
  • Maafisa usalama wa Somalia kupatiwa mafunzo zaidi na kikosi cha AMISOM

Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kimeazimia kuongeza kozi za mafunzo kwa maafisa usalama wa nchi hiyo ya pembe ya Afrika.

Christine Alalo, Kamishna Msaidizi wa Polisi wa kikosi cha AMISOM nchini Somalia amesema kuwa, lengo la kuongezwa zaidi kozi za mafunzo kwa maafisa usalama wa Somalia ni kujiandaa kwa ajili ya kusimamia vyema uchaguzi mkuu ujao nchini humo.

Polisi wa Somalia

Amesema kuwa, kikosi cha polisi cha Uganda na vikosi vingine vya Umoja wa Afrika vinavyohudumu nchini Somalia chini ya mwavuli wa kikosi cha kusimamia amani nchini humo AMISOM vitavisaidia vikosi vya usalama vya nchi hiyo kusimamia amani wakati wa kufanyika uchaguzi huo Septemba na Oktoba mwaka huu.

Aidha Christine Alalo, Kamishna Msaidizi wa Polisi wa kikosi cha AMISOM nchini Somalia ametaka kuweko ushirikiano zaidi kati ya vikosi hivyo na polisi ya Somalia kwa ajili ya kukabiliana na tishio la wanamgambo wa al-Shabab.

Amesema, moja ya majukumu ya kikosi cha AMISOM nchini Somalia ni kuinua kiwango cha uwezo wa kikosi cha polisi ya nchi hiyo.

Wanamgambo wa al-Shabab ambao ni tishio kwa usalama wa Somalia

Nchi ya Somalia iliyoko katika Pembe ya Afrika imekuwa ikikabiliwa na machafuko kwa miaka kadhaa sasa huku kundi la wanamgambo wa al-Shabab likitishia pakubwa usalama wa nchi hiyo na hata wa nchi jirani.

Mbali na ukosefu wa usalama, Somalia imekuwa ikikabiliwa na tatizo kubwa la ukame na baa la njaa hali ambayo imewafanya baadhi ya raia kuikimbia nchi hiyo na kuomba hifadhi katika nchi jirani.